RAIS WILLIAM RUTO ATOA ONYO JUU YA MAANDAMANO


 

Rais William Ruto ametoa onyo kali kuhusu maandamano ya Azimio yaliyopangwa kufanyika siku ya Jumatano.

Akizungumza mjini Ruai Jumanne, Rais alithibitisha kwamba hataruhusu maisha ya Mkenya yeyote kupotea kutokana na maandamano.

"Walifanya maandamano, na Wakenya wasita wakapoteza maisha yao. Mnataka maandamano ifanyike, maisha mengine yapotezwe? Haitatokea," Ruto alisema.

Ili kujiepusha, Ruto alisema kuwa hataruhusu kifo chochote kutokana na kuridhika kwa mtu kisiasa.

Kiongozi huyo aliambia upinzani kukubali matokeo ya uchaguzi wa Agosti 2022 na kuendelea.

"Iwapo unataka uchaguzi mwingine, subiri ratiba ya IEBC kuhusu lini uchaguzi mkuu ujao utafanyika. Ni wakati wa kufanya kazi," aliongeza.

Kinara wa upinzani Raila Odinga aliapa kuwaongoza wafuasi wake barabarani kwa maandamano dhidi ya serikali siku ya Jumatano.

Maandamano hayo yanatarajiwa kufanyika katika miji mikuu ya nchi huku Raila akiwa tayari amewatuma wanachama wakuu wa muungano wa Azimio kuongoza maandamano hayo katika ngazi za mashinani.

Maandamano ya Saba Saba ya siku ya Ijumaa iliyopita yalishika kasi huku sehemu mbalimbali za nchi zikiwemo Kisumu, Mombasa, Kisii, Kakamega, Kirinyaga, Machakos na Nyahururu zikishiriki.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne jioni, Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome alisema viongozi wa muungano wa Azimio unaoongozwa na Raila Odinga hawajawasilisha taarifa yoyote rasmi kwa polisi kuhusu maandamano yaliopangwa, kwa hivyo mikusanyiko hiyo itachukuliwa kuwa haramu.

Kwa hivyo IG ya Polisi imeapa kutumia "njia zote halali" kutawanya mikusanyiko yoyote ambayo itafanyika Jumatano.

Maandamano hayo, kwa mujibu wa muungano wa Azimio, ni sehemu ya kushinikiza Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua kuondoka afisini kwa msingi kuwa wameshindwa kutanguliza masaibu ya Wakenya na badala yake kutunga sheria za kutoza ushuru.

Odinga ambaye alifanya mkutano wa mazungumzo ya umma katika soko la Kenyatta jijini Nairobi siku ya Jumanne amewataka Wakenya bila kujali itikadi zao za kisiasa kujitokeza kwa wingi Jumatano na kujiunga na maandamano.

Post a Comment

0 Comments