DKT MABULA AHAMASISHA UJENZI WA NYUMBA ZA WATUMISHI

Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Waziri wa wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi MNEC Mhe Dkt Angeline Mabula amewaahidi wananchi wa mtaa wa Chasubi kata ya Kayenze matofali yote yatakayohitajika katika ujenzi wa nyumba za walimu mara baada ya wananchi kukamilisha ujenzi wa misingi ya nyumba hizo kama sehemu ya kuhamasisha ujenzi wa nyumba kwa watumishi.  
Hayo ameyabainisha wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi, kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kukagua miradi inayotekelezwa kwa fedha za mfuko wa jimbo na fedha za Serikali kuu ambapo amewapongeza kwa namna wanavyochangia na kushiriki shughuli za maendeleo
‘.. Niwapongeze kwa juhudi zenu za kuchangia maendeleo na mie kama mwakilishi wenu niwaahidi anzisheni misingi ya nyumba za walimu mie nitawapa matofali kisha meya atamalizia ..’ Alisema
Aidha Dkt Mabula amemshukuru Rais Mhe Samia Suluhu Hasan kwa fedha anazozitoa kwaajili ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Jimbo la Ilemela ambapo zaidi ya Bilioni 52 zimeshatolewa mpaka sasa
Kwa upande wake katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Hasan Milanga amewataka viongozi wa CCM ngazi ya mitaa, kata na wilaya kutokuwa madalali na watia hofu kwa viongozi waliopo madarakani kwa kushiriki mchezo mchafu wa kuanza kampeni kabla ya wakati huku akisisitiza wenyeviti wa Serikali za mitaa na madiwani kufanya mikutano na kueleza kazi nzuri zinazofanywa na Serikali
Nae mstahiki meya wa manispaa ya Ilemela Mhe Renatus Mulunga mbali na kumpongeza mbunge wa Jimbo hilo kwa namna anavyoshiriki utekelezaji wa maendeleo ndani ya Jimbo lake, Ameahidi kuunga mkono ukamilishaji wa miradi yote itakayoanzishwa kwa nguvu za wananchi
Simon Joseph ni mwananchi wa kata ya Shibula yeye amepongeza utaratibu wa mbunge huyo wa kufanya ziara ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi kila mara linapokwisha bunge la bajeti na kabla kwani kufanya hivyo kunasaidia kupunguza kero na changamoto za wananchi.

Post a Comment

0 Comments